Ikolojia ya mjini

Kuimarisha bayoanuai kwa kutumia usanifu wa Gradient Canopy kimandhari.

Dakika 3

Maua mekundu ya nafaka inayofanana na ngano pamoja na miti ya gome nyekundu ya pasifiki katika Gradient Canopy. Picha: Mark Wickens.

Kudumisha mazingira ya tawi ambayo ni bora kiikolojia kuna manufaa, si tu kwa sayari yetu, bali pia kwa watu. Mifumo ikolojia na mandhari bora yenye uanuai hukuza bayoanuai, huongeza ustahimilivu wa kiikolojia na yana manufaa makubwa kwenye afya ya binadamu. Kwa sababu hii, muundo wetu wa Gradient Canopy unalenga kujenga upya mifumo ikolojia yenye bayoanuai katika eneo hilo.

Kwenye eka nne za Gradient Canopy zenye mimea, tulijitahidi kukuza upya vipengee vya mfumo ikolojia ambavyo zamani vilipatikana kwa wingi katika eneo la Silicon Valley, ikiwa ni pamoja na misitu ya mialoni, vijisitu vya miti inayomea karibu na maji, vichaka na nyasi. Kwa kiwango kikubwa, mandhari yana spishi za asili, ikiwa ni pamoja na takribani miti 400 ya asili na mimea ya asili inayovutia wadudu wanaochavua, kama vile maua ya kipepeo (milkweed), maua ya yarrow na sage. Lengo ni kurudisha turathi za kiikolojia za eneo hilo na kuimarisha maisha ya binadamu, huku tukidumisha mandhari bora ya kuvutia yanayofaa mkusanyiko bayoanuai wa spishi.

Maua ya yarrow na mnanaa wa coyote katika Gradient Canopy

Maua ya yarrow na mnanaa wa coyote katika Gradient Canopy. Picha: Mark Wickens.

Sehemu muhimu ya mkakati wetu wa kiikolojia katika Gradient Canopy unalenga zaidi aina moja mahususi ya miti: mialoni. Mialoni, ambayo ni maarufu katika mandhari ya California, wakati mmoja ilipatikana kwa wingi sana kwenye eneo la Silicon Valley. Mialoni ya asili ina uwezo wa kustahimili ukame, moto na ina ufanisi zaidi katika kuondoa uchafuzi wa hewa na kufyonza kaboni kwenye angahewa. Pamoja na hayo, mifumo ikolojia ya misitu ya mialoni ni makao ya wanyama na mimea anuai katika eneo la California, ikiwa na spishi 2,000 za ziada za mimea na takribani spishi 5,000 za wadudu. Mamia zaidi ya ndege, mamalia na wanyamapori wengine hutegemea mandhari ya misitu ya mialoni kupata chakula, kivuli na mahali pa kujisitiri.

Tulishirikiana na wanasayansi wa eneo hili kusanifu safu ya miti iliyounganishwa ili kupata mandhari yanayojumuisha mialoni, pamoja na spishi nyingine za miti ya asili, kama vile buckeye, mikuyu na miti inayomea karibu na maji. Safu ya miti iliyounganishwa huwapa wanyamapori ushoroba wa kupitia katika mazingira yaliyojengwa na hupunguza athari ya ongezeko la joto katika maeneo ya mjini.

Mimea ya asili inayofaa wadudu wanaochavua inamea chini ya miti ya asili ya Gradient Canopy na inavutia vipepeo, ndege na nyuki wa eneo hilo. Sehemu ya mandhari imeundwa ili kuwasaidia vipepeo wakubwa wa magharibi, kwa kutumia mbinu bora inayopatikana ya kisayansi kuunda mchanganyiko sahihi wa mimea ya maua ya kipepeo (milkweed), inayowasaidia viwavi na mayai ya vipepeo wa magharibi na maua, ambayo huwapatia vipepeo wanaopita nguvu katika safari yao ya uhamaji.

Katika Gradient Canopy, tumechanganya mimea ya asili inayovutia wadudu wanaochavua pamoja na vitalu vilivyolimwa na mizinga ya nyuki wa asali ili kufanikisha Agizo la Kilimo cha Mjini la Living Building Challenge, linalokusudiwa kuhakikisha kwamba jamii inapata vyakula bora vinavyopandwa karibu. Vitalu viwili vinazalisha vyakula vya migahawa na vyumba vya upishi vya WanaGoogle na vinaonyesha jinsi mandhari ya asili na kilimo vinaweza kufanya kazi pamoja ili kuzalisha vyakula katika eneo hilo.

Kitalu cha bustani katika Gradient Canopy.

Kitalu cha bustani katika Gradient Canopy.

Pia tulishirikiana na The Planet Bee Foundation, shirika lisilolenga faida linalosimamia mizinga ya nyuki ya Google jijini Mountain View, ili kuweka mizinga mitatu ya nyuki wa asali katika eneo. Kama sehemu ya mchakato wetu wa kusanifu, tulifanya utafiti kuhusu jinsi mandhari yanavyoweza kusaidia nyuki wa asali wasio wa asili na nyuki wa asili kukuza faida za wote wawili. Utafiti huu utabaini jinsi Google itakavyojumuisha nyuki wa asali wasio wa asili katika mandhari ya kiikolojia ya asili siku zijazo ili kunufaisha bayoanuai ya asili pamoja na uzalishaji wa vyakula katika eneo hilo.

Muundo wa ikolojia ya mji wa Gradient Canopy umeongozwa na mpango wa ikolojia wa Google, ambao tulizindua mwaka wa 2014 ili kujumuisha mbinu bora zaidi za sayansi zilizopo katika usanifu wa sehemu zetu za nje. Hakika, Gradient Canopy ni sehemu moja muhimu ya maono yetu makubwa ya kuimarisha mazingira na bayoanuai kupitia matawi yetu.