Njia ya kuwa na mustakabali safi na unaojali afya inaanzia katika uamuzi mdogo tunaofanya kila siku. Ndiyo maana mara kwa mara tunatafuta njia za kuwa na manufaa chanya katika mazingira na kuwajibika zaidi katika matumizi yetu ya nishati, maji na mali nyingine asili. Hapa Gradient Canopy, ndiyo maana tuliamua kujenga jengo hili kwa kuzingatia kanuni za muundo wa duara, zinazosaidia kupunguza mahitaji ya mali asili zenye kikomo. Muundo wa duara unalenga kuendeleza matumizi ya nyenzo kwa muda mrefu kadiri inavyowezekana, ndiyo maana tulijumuisha nyenzo nyingi zilizookolewa kwenye jengo hili.
Hapa Gradient Canopy, tuliweka zaidi ya bidhaa 30 kutoka kwenye vyanzo vilivyookolewa katika jengo zima. Bidhaa hizi ni pamoja na chanja za baiskeli, makabati, mazulia, vigae na mbao zilizookolewa ambazo huenda zingetupwa jalalani. Kujumuisha nyenzo zilizookolewa katika kiwango hiki kulisaidia jengo hili kupata cheti cha Kiwango cha Nyenzo kwenye Living Building Challenge (LBC) kutoka taasisi ya International Living Future Institute (ILFI), inayolenga kusaidia kuunda uchumi wa nyenzo zisizo na sumu, unaorejesha mfumo ikolojia na wenye uwazi.
Kwa sababu ya ukubwa wa jengo, ilitupasa tubuni mikakati kadhaa ili kupata nyenzo zilizookolewa katika kiwango kinachofaa. Kwa mfano, kupata nyenzo kama mazulia au vigae vilivyookolewa ilikuwa ngumu kwa sababu muundo huo ulihitaji nyenzo nyingi zaidi na ilifaa kuwa na ulinganifu katika ukubwa, rangi na ubora katika jengo zima.
Mkakati muhimu tuliotumia ni kutumia tena vitu kutoka kwenye nyenzo tulizohifadhi katika bohari hapa Google. Hii inamaanisha kuwa tulitafuta katika vitu tulivyohifadhi kwenye dari yetu, ikiwa ni pamoja na nyenzo nyingine mpya ambazo hazikutumika kwenye miradi iliyotangulia na vitu vilivyoondolewa katika majengo kabla ya kubomolewa. Kwa kutafuta katika vitu ambavyo tayari tulikuwa navyo, tuliweza kujumuisha vigae vya mazulia, chanja za baiskeli, vigae vya kauri pamoja na vigae vya dari vya akustika vilivyookolewa.
Njia nyingine tuliyotumia kujumuisha nyenzo zilizookolewa ni kwa kutumia mbao zilizookolewa kutoka vyanzo mbalimbali katika maeneo ya karibu. Kwa mfano, tulitumia mbao zilizoondolewa wakati wa ujenzi kuunda viti vinavyopatikana kila sehemu ya jengo. Pia tulitafuta wauzaji katika eneo walete mbao zilizookolewa, ambazo zilitumika kwa vitu kama vile kuweka paneli za ukuta katika maeneo ya kuegesha baiskeli na kuweka sakafu kwenye Google Store.