Kwenye Google Visitor Experience katika tawi la Gradient Canopy, kipengele muhimu cha utamaduni wa Google kitapatikana kwa umma kwa mara ya kwanza: mpango wetu wa chakula. Cafe @ Mountain View mpya ni huduma yetu ya kwanza kabisa ya chakula inayolenga umma, inayoruhusu jamii inunue chakula na kushiriki katika vipaumbele na mwongozo wetu wa utunzaji wa mazingira katika mchakato wa kusaidia ulimwengu.
Tangu 1999, mpango wetu wa chakula umechangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza utamaduni wa Google wa ubunifu, ushirikiano na jamii. Kwa kutoa huduma za vyakula vitamu vyenye virutubishi katika maeneo ya kuvutia, tunajitahidi kuwezesha mahusiano ya wanadamu na ubadilishanaji wa mawazo. Vyakula vyetu vimehamasisha huduma nyingi za ubunifu — ikiwemo Gmail, ambayo ilitokana na mazungumzo yaliyofanyika katika moja ya mikahawa yetu wakati wa chakula cha mchana.
Mpango wa Google wa chakula unalenga jamii kila wakati, kwa kuijenga katika matawi yetu na kuunganisha na maeneo yetu mapana kupitia vyanzo na uandaaji wa vyakula. Mojawapo ya kanuni zetu kuu za mapishi ni kuilinda jamii, kumaanisha kwamba tunaelewa kuwa uamuzi tunaofanya kuhusu vyakula una matokeo chanya ndani ya Google na kwingineko. Iwe ni katika menyu tunazounda, sehemu tunakonunua vyakula vyetu au namna tunavyoviandaa, kila mara tunafikiria jinsi mpango wetu wa chakula unavyoweza kuwa na manufaa katika mifumo wa usambazaji kwenye maeneo ya karibu na katika sayari yetu kwa ujumla.
Mpango wetu wa chakula unaongoza ushirika wa kimkakati na mipango ya utunzaji wa mazingira ili kuchochea mabadiliko chanya na kuweka misingi ya mifumo bora ya chakula siku zijazo. Wapishi wetu huandaa vyakula kutokana na viungo vya msimu kutoka maeneo ya karibu, mchakato unaowezeshwa na uhusiano tulionao na wasambazaji wa maeneo hayo. Tunakagua kwa makini wasambazaji wa viungo na kushirikiana na wale wanaozingatia maadili yetu, ikiwa ni pamoja na utunzaji wa mazingira, umiliki wa biashara mbalimbali na uboreshaji wa jamii. Ili kupunguza jumla ya kaboni, tunawapatia kipaumbele wasambazaji wanaojihusisha na kilimo endelevu, kutumia bidhaa upya kwa ubunifu na ufungashaji mdogo na kuchagua bidhaa za maeneo ya karibu badala ya zilizosafirishwa kwa ndege inapowezekana. Kwa njia hii, tunaendeleza sekta ya chakula na vinywaji tukiangazia vitendo vya uwajibikaji ambavyo ni bora kwa mazingira na jamii zinazotulea.
Kando na kutafuta viungo, tunalenga mbinu mbili muhimu za utunzaji wa mazingira katika mpango wetu wa chakula: kupunguza taka za vyakula na kuondoa plastiki zinazotumika mara moja. Tunafahamu kuwa takriban asilimia 35 ya vyakula vinavyozalishwa ili kuliwa na binadamu au takriban ratili bilioni 133 za vyakula huharibiwa kila mwaka. Ili kuwezesha malengo ya Google ya utunzaji wa mazingira, tunalenga kuacha kutupa taka za vyakula majalalani kufikia 2025. Vipi? Tuna mbinu yenye sehemu tatu inayolenga kuzuia uharibifu wakati wa kupata na kununua vyakula, kuboresha majiko na migahawa yetu kwa kutumia teknolojia ili kupunguza taka katika shughuli zetu za jikoni na kuhakikisha kwamba chakula kinachobaki kinatumika kwa madhumuni mengine au kutupwa inavyofaa. Kuanzia 2014 hadi 2021, tulizuia takriban ratili milioni 10 za chakula kutupwa katika majalala.
Pia, tunajitahidi kupunguza plastiki katika sehemu za vyakula. Tunanunua kwa wingi na kuchagua bidhaa zilizofungashwa kidogo na kwa ubunifu inapowezekana na tumeanza kutekeleza matumizi ya vizimba vya waya kusafirisha bidhaa. Pia tuliangalia jinsi tunavyoweza kutumia mandhari mapya ya baa ya mtindi badala ya vikombe vya mtindi vinavyotumika mara moja na kutoa vitafunwa katika vyombo vya kuhifadhia vitu vingi ili kutoweka vifungashio vinavyotumika mara moja katika mifumo ya taka.